Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa kishahidi kwa Imam Hasan al-Askari (as), tunawaletea wasomaji wapendwa muhtasari wa wasifu wa Imam wa kumi na mmoja na baba yake Mtukufu Imam wa Zama (aj).
Swali:
Maisha ya Imam Hasan al-Askari (as) yaliambatana na vipindi na misukosuko gani?
Jibu kwa muhtasari:
Imam wa kumi na mmoja wa Mashia alizaliwa mwaka 232 Hijria. Baba yake alikuwa Imam Hadi (as), na mama yake alikuwa mwanamke mchamungu na mwema aliyeitwa “Sawsan”.
Kwa amri ya Khalifa wa Bani Abbas, alilazimishwa kuishi Samarra, katika eneo la “Askari”; kwa sababu hiyo aliitwa al-Askari.
Alikuwa na umri wa miaka 22 wakati baba yake mtukufu alipouawa kishahidi, na muda wa Uimamu wake ulikuwa miaka 6. Mwaka 260 Hijria, akiwa na umri wa miaka 28, aliuawa kishahidi na akazikwa katika nyumba yake huko Samarra, kando ya kaburi la baba yake.
Katika kipindi kifupi cha Uimamu wake, alikuwa zama moja na Makhalifa watatu wa Bani Abbas: al-Mu'tazz Billah, al-Muhtadi Billah na al-Mu'tamid Billah.
Jibu kwa ufafanuzi:
Imam al-Askari, Imam wa kumi na mmoja wa Mashia, alizaliwa mwaka 232 Hijria.¹ Baba yake alikuwa Imam wa kumi, Hadhrat Hadi (as), na mama yake alikuwa mwanamke mchamungu na mwema aliyeitwa “Hudaytha”;² baadhi ya vyanzo vimemtaja kwa jina la “Sawsan”.³
Mama huyu mtukufu alikuwa miongoni mwa wanawake wema na wenye uelewa wa mafundisho ya Kiislamu. Na inatosha kuwa ni dalili ya ubora wake kwamba baada ya kuuawa kishahidi kwa Imam Hasan al-Askari (as), alikuwa kimbilio na tegemeo la Mashia katika kipindi hicho kilichokuwa na mzozo mkubwa na hofu nyingi.⁴
Kwa kuwa Imam wa kumi na mmoja, kwa amri ya Khalifa wa Bani Abbas, alilazimishwa kuishi Samarra, katika eneo la “Askari”, kwa sababu hiyo aliitwa “al-Askari”.⁵
Miongoni mwa lakabu zake mashuhuri nyingine ni “Naqi” na “Zaki”,⁶ na kuniya yake ni “Abu Muhammad”.
Alikuwa na umri wa miaka 22 wakati baba yake mtukufu alipouawa kishahidi. Muda wa Uimamu wake ulikuwa miaka 6, na umri wake mtukufu ulikuwa miaka 28. Mwaka 260 Hijria aliuawa kishahidi na akazikwa katika nyumba yake huko Samarra, kando ya kaburi la baba yake.⁷
Imam al-Askari (as), katika kipindi kifupi cha Uimamu wake, alikuwa zama moja na Makhalifa watatu wa Bani Abbas, ambao kila mmoja wao alikuwa dhalimu kuliko aliyemtangulia, makhalifa hao ni:
1 – Al-Mu'tazz Billah (252–255 Hijria)
2 – Al-Muhtadi Billah (255–256 Hijria)
3 – Al-Mu'tamid Billah (256–279 Hijria)
Makhalifa wa Bani Abbas, ambao mwanzoni waliinuka kwa madai ya kuwaunga mkono Alawiyyin na kulipiza kisasi kwa ajili yao dhidi ya Bani Umayya, walipuuza yale waliyokuwa wamewaahidi watu hapo awali. Badala yake, walianza kufanya dhuluma na kutawala kwa mabavu, kama walivyofanya Makhalifa wa Bani Umayya, na hata wakazidi kuwa dhalimu na watawala wa mabavu kuliko wao.⁸
Rejea:
(1). Al-Kulayni, Usul al-Kafi, Tehran, Maktaba al-Saduq, 1381 Hijria, juzuu ya 1, uk. 503; Sheikh Mufid, Al-Irshad, Qum, Maktaba Basirati, uk. 335; Ibn Shahr Ashub, Manaqib Aal Abi Talib, Qum, Makta Mustafa, juzuu ya 4, uk. 422; Tabarsi, A'lam al-Wara, chapa ya tatu, Tehran, Dar al-Kutub al-Islamiyya, uk. 367. Mas'udi na Ali bin Isa Arbili wametaja kuwa kuzaliwa kwa Hadhrat huyo ilikuwa mwaka 231 Hijria.
(2). Sheikh Mufid, kitabu hicho, uk. 335; Tabarsi, kitabu hicho, uk. 366.
(3). Al-Kulayni, kitabu hicho, uk. 503; Ali bin Isa Arbili, Kashf al-Ghumma, Tabriz, Maktaba Bani Hashimi, 1381 Hijria, uk. 192.
(4). Wakanat min al-arifati al-salihat, wa kafa fi fadliha annaha kanat mafza'a al-shi'a ba'da wafati Abi Muhammad. (Haj Sheikh Abbas Qummi, Al-Anwar al-Bahiyya, Mashhad, Maktaba Ja'fari, uk. 151).
(5). Swaduq, Ilal al-Shara'i, Qum, Maktaba al-Tabataba'i, juzuu ya 1, mlango wa 176, uk. 230; vilevile Saduq, Ma'ani al-Akhbar, Tehran, Maktaba al-Saduq, Mu'assasa Dar al-Ilm, 1379 Hijria, uk. 65.
(6). Abu Ja'far Muhammad bin Jarir al-Tabari, Dala'il al-Imama, chapa ya tatu, Qum, Manshurat al-Radhi, 1363 Hijria ya Shamsia, uk. 223.
(7). Sheikh Mufid, Al-Irshad, Qum, Maktaba Basirati, uk. 345; Sheikh Abdullah al-Shabrawi, Al-Ithaf bi Hubb al-Ashraf, chapa ya 2, Qum, Manshurat al-Radhi, 1363 Hijria ya Shamsia, uk. 178–179.
(8). Imekusanywa kutoka katika kitabu: Sirat-e Pishvayan, Mahdi Pishvaei, Taasisi ya Imam Swadiq (as), Qum, 1390 Hijria ya Shamsia, uk. 615.
Maoni yako